Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakiwa katika mazoezi huko Monduli, Arusha. Jeshi hilo litaadhimisha miaka 52 ya kuanzishwa kwake Septemba Mosi kwa kufanya usafi katika mitaa mbalimbali ya nchi. |
Mengine
mawili ni maadhimisho ya miaka 52 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) ambayo yataambatana na kufanya usafi katika mitaa
mbalimbali nchini huku kukiwa na tangazo la Chadema la kufanya
maandamano na mikutano isiyo na kikomo nchini katika kile chama hicho
cha upinzani kilichoeleza kuwa ni operesheni ya Umoja wa Kupinga
Udikteta Tanzania (UKUTA) ambayo hata hivyo, imezuiwa na Jeshi la
Polisi.
Chadema kimekuja na operesheni hiyo kikidai
kwamba hatua kauli ya Rais John Magufuli kuzuia shughuli za kisiasa za
majukwaani hadi mwaka 2020 ni ukandamizaji wa haki na demokrasia.
Kauli
hiyo ya Chadema iliungwa mkono na vyama vyenye uwakilishi bungeni
ambavyo mwishoni mwa wiki iliyopita vilitoa msimamo wa pamoja vikisema
kwamba iwapo Rais hapendi kukosolewa, apeleke bungeni muswada wa hati ya
dharura wa kufuta vyama vyote vya siasa nchini, kauli iliyotolewa siku
moja tangu Jeshi la Polisi kupiga marufuku mikutano ya ndani ya kisiasa
kwa madai kuwa ina lengo la kupanga uchochezi.
Baadhi
ya wanachama na viongozi wa Chadema wamekamatwa maeneo mbalimbali nchini
na baadhi kufikishwa mahakamani kwa madai ya kutoa kauli za uchochezi. Mvutano
huo kati ya polisi na Chadema umewalazimu viongozi mbalimbali wa dini
kufanya mikutano kadhaa ya usuluhishi na kuitaka Serikali na Chadema
kuifikiria amani ya Tanzania kwa kutafuta njia muafaka za kumaliza
tofauti hizo.
Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu, Abubakar
Zubeir alitaka madai ya Chadema yasipuuzwe, bali yasikilizwe na yapatiwe
ufumbuzi badala ya kutumia nguvu kuyapuuza huku Mkuu wa Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Frederick Shoo akieleza kuwa
hali wanayoiona haiwafurahishi hata kidogo.
Juzi, Rais
Magufuli alikutana ana kwa ana na aliyekuwa mgombea urais wa Chadema na
Ukawa, Edward Lowassa na kupeana mikono, katika maadhimisho ya miaka 50
ya ndoa ya Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na mkewe Anna. Kitendo
cha mahasimu hao waliochuana vikali katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25
mwaka jana, kupeana mikono kinazidi kuibua maswali mengi na tafsiri ya
tukio la maandamano na mikutano ya hadhara litakalofanywa na Chadema.
MAADHIMISHO JWTZ
Siku
hiyo pia JWTZ itaadhimisha miaka 52 ya kuanzishwa kwake kwa kufanya
usafi kwenye maeneo mbalimbali huku jeshi hilo likieleza kuwa
halitafanya maandamano kwa kuwa Serikali imeyazuia.
Jeshi
hilo liliundwa upya Septemba 1964 baada ya kuvunja lile lililorithiwa
kutoka ukoloni la Tanganyika Rifles ambalo liliasi Januari 20, 1964.
Msemaji
wa JWTZ, Kanali Ngemela Lubinga alisema shughuli ya kufanya usafi
pamoja na upandaji miti, itafanyika katika maeneo mbalimbali nchini hadi
siku ya kilele cha maadhimisho hayo. Pia, wanajeshi watajitolea damu
katika hospitali za jeshi. Kadhalika, madaktari wa JWTZ
watatoa huduma za tiba bure kama upimaji wa virusi vya Ukimwi, kisukari
na shinikizo la damu na kushiriki michezo mbalimbali baina yake,
taasisi mbalimbali.
KUPATWA KWA JUA
Tukio
la kupatwa kwa jua litakalodumu kwa takriban saa mbili, ni la aina yake
kwa kuwa hutokea kwa nadra na baadhi ya dini zinawataka waumini wake
wakati wa kipindi hicho kuwa kwenye swala maalumu. Watu
wanaoishi katika ukanda wenye upana wa kilomita 100 unaokatisha Kusini
mwa Tanzania, kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) kuelekea
Katavi, Mbeya, Ruvuma hadi Masasi na kuingia Msumbiji, siku hiyo wataona
jua kama duara jembamba mithili ya pete, kwa vile asilimia 98 ya jua
katika maeneo yao litakuwa limejificha nyuma ya mwezi.
Wataalamu
wameeleza kuwa wananchi wanaweza kushuhudia kupatwa kwa jua kwa usalama
kwa kutumia miwani maalumu ya mwanga wa jua. Wapo
ambao wataitumia siku hiyo kujifunza sayansi ili kuelewa kwa nini
kinatokea kile watakachokiona, tukio linaloweza kutumiwa na shule na
taasisi za elimu kuendeleza sayansi na kuvutia wanafunzi.
Bodi
ya Utalii Tanzania (TTB) imesema tukio hilo litafungua milango kwa
sekta ya utalii katika Nyanda za Juu Kusini kwa kuwa watalii na watafiti
kutoka ndani na nje ya nchi watembelea maeneo hayo kushuhudia tukio
hilo la kipekee duniani. Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji
wa TTB, Philip Chitaunga alisema Bodi hiyo imeandaa safari ya watu 50
itakayowajumuisha wanahabari na watu maarufu nchini kwa ajili ya
kushuhudia tukio hilo la kihistoria.
“Sekta ya utalii
ndiyo inayoongoza kuiingizia nchi pato la kigeni… hivyo tukio hili
tunaliona kama ni fursa itakayoutangaza utalii wa Kusini. Kusini kwa
sasa miundombinu ni mizuri, kuna uwanja mkubwa wa ndege, barabara
zinapitika, hivyo Tanzania itafahamika zaidi,” alisema Chitaunga.
WAZIRI MKUU KUHAMIA DODOMA
WAZIRI MKUU KUHAMIA DODOMA
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa kuhamia Dodoma ni miongoni mwa matukio
yatakayotikisa Septemba Mosi, ikiwa ni utekelezaji wa kauli ya Rais
Magufuli ya kutaka Serikali kuhamia mjini humo baada ya jambo hilo
kushindikana tangu kutangazwa kwake miaka ya 70. Julai
24 mwaka huu, Majaliwa alieleza dhamira yake ya kuhamia Dodoma ifikapo
Septemba ili kuonyesha kuwa Serikali imedhamiria kutekeleza ahadi
inazotoa kwa wananchi.
Alitoa kauli hiyo wakati
akizungumza na mamia ya wakazi wa Dodoma na kuwashukuru kwa ushiriki wao
kwenye maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa zilizofanyika kwa
mara ya kwanza kwenye Uwanja wa Mashujaa, mjini humo. Akizungumzia
tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christina Mndeme amewataka
wananchi kujitokeza kwa wingi siku hiyo kumpokea Waziri Mkuu. “Maandalizi
yanaendelea vizuri na ninawaomba wakazi wa Dodoma kujitokeza kwa wingi
kumpokea Waziri Mkuu kwa sababu hili ni tukio la kihistoria.”
No comments:
Post a Comment
Subscribe My YouTube Channel Here:
https://www.youtube.com/channel/UCRdp...
Like My Facebook page:
https://www.facebook.com/lyizzmaker
Follow Me On Twitter:
https://www.twitter.com/habariyamjini
Follow Me on Instagram:
https://www.instagram.com/habariyamjini