Monday, 21 November 2016

YALIYOTIA DOA UTAWALA WA JPM.


Serikali ya Awamu ya Tano imefanya vizuri katika mwaka wake wa kwanza, ikifanikiwa kurejesha nidhamu ya kazi kwa kiasi kikubwa, kupambana na ufisadi, kukusanya mapato ya Serikali na kuwawajibisha bila aibu viongozi na watumishi wa umma.

Ununuzi wa ndege mbili, malipo yaliyofanikisha awamu ya pili ya mradi wa umeme wa Segerea, kuanzisha mahakama ya mafisadi, kuzuia matumizi yasiyo ya lazima kwa kufuta sherehe za maadhimisho ni kati ya mambo yaliyofurahiwa na wengi.


Lakini, wakati Rais John Magufuli na Serikali yake wakianza mwaka wa pili, baadhi ya wasomi na wanasiasa wamemshauri Rais Magufuli afanyie kazi mambo 10, likiwamo la mchakato wa Katiba mpya ambalo alisema si kipaumbele chake.

Mbali ya Katiba, wachambuzi hao walitaja mambo mengine muhimu yanayopaswa kufanyiwa kazi kuwa ni kuangalia uwezekano wa kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera, hali ya siasa Zanzibar, kuheshimu sheria wakati wa kuwajibisha watumishi, kuruhusu uhuru wa mihimili ya nchi, kuruhusu demokrasia, kuruhusu shughuli zote za Bunge kuonyeshwa moja moja na vituo vya televisheni na redio na kuepuka kauli tata.

“(Rais Magufuli) Amefanikiwa katika mapambano dhidi ya rushwa, kuwafanya watu wapende na kuheshimu kazi. Sasa atakavyomaliza na kuondoka, haya yote yataachwa ikiwa hatasimamia mchakato wa Katiba mpya,” alisema mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu, Dk Hellen Kijo-Bisimba.

Katiba Mpya
Ilani ya CCM inazungumzia mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa shughuli za Serikali kwa kipindi cha 2010-2015 kuwa ni pamoja na mchakato wa kuandika Katiba mpya kuendeshwa na kufikia hatua ya kupigia kura Katiba Inayopendekezwa baada ya kupitishwa na Bunge maalumu.
Akipokea ripoti ya Uchaguzi Mkuu Juni 23, Magufuli alisema mambo fulani yataongezeka katika Katiba Inayopendekezwa, lakini Novemba 4 alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari alisema hakuwahi kuzungumzia Katiba wakati wa kampeni zake kwa hiyo si kipaumbele chake, na kwamba anachotaka kwanza ni “kunyoosha nchi”, kauli inayotafsiriwa kuwa ni kuisigina Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Kushughulikia maafa ya Kagera
Suala jingine ambalo wachambuzi wamelizungumzia ni jinsi Serikali ilivyoshughulikia tetemeko la ardhi lililoikumba mikoa ya Kanda ya Ziwa na hasa, Kagera ambako takribani watu 17 walipoteza maisha, zaidi ya nyumba 840 kubomoka na nyingine 1,264 kuharibika.
Kutokana na janga hilo, Septemba 11, Rais Magufuli aliahirisha ziara ya siku tatu nchini Zambia ambako pamoja na mambo mengine, angehudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Edgar Lungu.
Septemba 18 wakati akipokea taarifa ya maafa yaliyosababishwa na tetemeko hilo kutoka kwa Waziri Mkuu, iliyoeleza kuwa zilikusanywa Sh3.6 bilioni, Rais Magufuli alisema Serikali itarekebisha miundombinu iliyoharibiwa na tetemeko na kuwataka waliobomolewa nyumba, wajipange kuzirekebisha. Serikali ilizuia watu au taasisi kutoa misaada kwa waathirika, badala yake ikaagiza wapitie Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, ambaye hivi karibuni alikaririwa akisema kipaumbele itakuwa ni ujenzi wa miundombinu na taasisi za serikali.

Maamuzi ya haraka
Serikali inadaiwa kuwajibisha wakuu wa idara kabla tuhuma dhidi yao kuthibitishwa. Baadhi yao walisimamishwa au kufukuzwa kazi katika mikutano ya hadhara na wengine wakati wanaendesha vikao. Jambo hili limekuwa likifanywa hata na wakuu wa mikoa na wilaya kwa kuwaweka mahabusu watu walio chini yao.

Kuzuia mikutano ya siasa
Dosari nyingine ni kutofuata Katiba, Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Utumishi wa Umma. Rais amezuia mikutano ya siasa na maandamano. Kwa kuwa Sheria hizo zinaruhusu, Jeshi la Polisi linatekeleza zuio hilo kwa maelezo kwamba ina viashiria vya kuvunja amani au kuibuka kwa magonjwa.
Pia, Waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma Na 1 wa mwaka 1992 uliorudiwa mwaka 2015 umewazuia askari kujihusisha na siasa, lakini wengi wamepewa nyadhifa za siasa.

Sakata la Zanzibar
Pia, hali ya kisiasa Zanzibar ni jambo jingine lililozungumzwa na wachambuzi. Wakati akilihutubia Bunge Novemba 20 mwaka jana, Rais Magufuli alionyesha uwezekano wa kuutafutia ufumbuzi mkwamo wa kisiasa Zanzibar na baadaye kuwa na mazungumzo na katibu mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad Desemba 21. Lakini hotuba mbili alizotoa katika ziara ya Pemba Septemba 2 na Unguja Septemba 3, Rais Magufuli aliondoa uwezekano wa kupatanisha makundi hasimu ya kisiasa kati ya CCM na CUF, jambo ambalo limekosolewa na wengi.
“Zanzibar imeathirika sana, yale matumaini ya kuweka mfumo mpya kupitia Katiba Mpya ya Jaji Joseph Warioba yamepotea lakini hata mipango ya kuimarisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa imepotea,” alisema mwenyekiti wa Baraza la Katiba Zanzibar, Profesa Abdul Sherrif. “Uchaguzi Zanzibar umeacha mpasuko wa wananchi badala ya kuwaunganisha.”

Matamko ya ghafla
Jambo jingine lililogusa wengi ni kufuta sherehe za maadhimisho na baadhi katika dakika za mwisho. Mfano ni uamuzi wa kuzuia wakuu wa mikoa na wilaya, wakurugenzi na maofisa wengine kwenda Simiyu kuhudhuria hafla ya kuzima Mwenge wa Uhuru, wakati baadhi walishafika na wengine wakiwa safarini.
Rais Magufuli aliwaambia maofisa wote waliofika Simiyu au waliokuwa njiani kurudi katika vituo vyao vya kazi na kurejesha fedha walizotumia.
Pia, Rais amekuwa akitoa kauli zinazodaiwa tata ambazo baadhi zinaweza kuwa na madhara kama kuwataka askari wa usalama barabarani kuondoa tairi za gari wanalokamata, au kuwapa polisi fedha za kubrashia viatu.

Bunge ‘live’
Suala jingine ni Bunge kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya shughuli za Bunge tofauti na ilivyokuwa katika Bunge la Tisa na la Kumi.

Kudhibiti mihimili
Ingawa Serikali ndiyo ina wajibu wa kutafuta fedha, Mahakama na Bunge ni mihimili inayojitegemea. Mwishoni mwa mwaka jana, Rais anadaiwa kuagiza fedha za sherehe ya kuwapongeza wabunge zitumike kununulia vitanda kwa ajili ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), na mapema mwaka huu, aliiomba mahakama imalize kesi za kodi ili Serikali ipate Sh1.4 trilioni na kuupa mhimili huo sehemu ya fedha hizo.

Mambo mengine
Mambo mengine ambayo yametajwa kutia doa mwaka mmoja wa Serikali ni nidhamu ya uoga kwa watumishi wa umma pamoja na kuyumba kwa hali ya kifedha miongoni mwa Watanzania jambo ambalo linaonekana kulalalamikiwa na makundi karibu yote.

Maoni ya wachambuzi
Wachambuzi waliohojiwa na gazeti hili kuhusu masuala hayo, walikuwa na maoni tofauti.
Dk Kijo-Bisimba, ambaye ni mwanasheria, alisema Katiba mpya ndiyo msingi wa kuwaongoza watawala kwa sababu inabeba yale yote ya msingi yanayotakiwa kutekelezwa bila kuvunja haki za binadamu.
“Rais ahakikishe Katiba mpya inapatikana, ile yenye maoni ya wananchi. Pia, awaache wanasiasa kwa sababu kitendo cha kuzuia mikutano kinawafanya wapate ya kuzungumza. Kama akiwaacha na yeye akasimamia Katiba na kutekeleza majukumu yake hawatapata jambo la kuzungumza,” alisema.
Mbunge wa Makete (CCM), Profesa Norman Sigalla alisema Rais Magufuli amefanya vizuri na kukifanya chama chake kiendelee kuaminika.
Hata hivyo, alisema ni vizuri aifanye Serikali yake iwapende matajiri wanaopata fedha zao kwa halali badala ya kuwaona fisadi.
“Baadhi ya wawekezaji wakisikia kwamba kila mwenye fedha Tanzania anaitwa fisadi, hawawezi kuja kuwekeza; vivyo hivyo matajiri hawawezi kuweka fedha kwenye mabenki yetu kwa sababu wanahofia kuonekana mafisadi,” alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili, Dk Ave Maria Semakafu alisifu utumbuaji wa majipu akisema umesaidia kuwashtua baadhi ya watendaji waliokuwa wakifanya kazi kwa mazoea.
Lakini alisema suala la Katiba mpya linapaswa kusubiriwa kwa muda badala ya kukurupuka.
Dk Semakafu alisema kilichokuwa kikipigiwa kelele zaidi kwenye Katiba ni viongozi kutowajibika na kukosa uadilifu, huku wachache wakinufaika na keki ya Taifa.
“Tuendelee kuona mwelekeo wa Rais Magufuli kwanza ndipo suala la Katiba lianze. Ikumbukwe kuwa kilichokosekana wakati ule ni suala usimamizi madhubuti ambao hivi sasa umeonekana,” alisema.
Kilio cha Dk Semakafu katika kipindi cha mwaka mmoja wa utawala wa Rais Magufuli ni suala la usawa wa kijinsia ambalo anasema nafasi za wanawake zimepungua, hasa katika ngazi za kufanya maamuzi.
“Idadi ya wanawake kwenye ngazi ya maamuzi imerudi nyuma, hili nalo litapaswa kupewa msukumo wa kikatiba muda utakapofika ili wanawake na wanaume wote kwa pamoja wahusike kwenye ngazi hii muhimu,” alisema.
Lakini mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa alisema Rais Magufuli ameonyesha kutovumilia kukoselewa.
Mchungaji Msigwa pia alisema kuzuia mikutano ya Bunge kuonyeshwa ‘live’, kuzuia mikutano ya hadhara ya siasa na kubana vyombo vya habari kunaashirisha kwamba hapendi kukoselewa.
“Maana yake ni kwamba wananchi wakifuatilia Bunge wataona hoja nzito zinavyojibiwa. Pia wanasiasa ndiyo wanaoweza kuzibua masikio ya Watanzania. Rais wetu hapendi kupata maoni na kukosolewa,” anasema.
Pia, alisema katika kipindi hicho Rais Magufuli ameonekana kushindwa kujibu kwa ufasaha maswali ya waandishi wa habari, jambo ambalo alisema ni udhaifu.
Hata hivyo, akizungumza na wahariri, Rais Magufuli alisema anapenda kukosolewa na anafanyia kazi ukosoaji hasa ule unaozingatia weledi.

No comments:

Post a Comment

Subscribe My YouTube Channel Here:
https://www.youtube.com/channel/UCRdp...

Like My Facebook page:
https://www.facebook.com/lyizzmaker

Follow Me On Twitter:
https://www.twitter.com/habariyamjini

Follow Me on Instagram:
https://www.instagram.com/habariyamjini