UHAKIKI unaoendelea kufanywa na Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), kujua uhalali wa wanaonufaika na mikopo hiyo, umeibua balaa kwa baadhi yao baada ya kuondolewa.
Hali hiyo inatokana na taarifa za HESLB kuonyesha kuwa hadi jana, tayari ya uhakiki huo ulikuwa umebaini kuwapo kwa wanafunzi 3,000 waliopata mikopo kimakosa kutokana na kupungukiwa vigezo, hivyo kuondolewa katika orodha ya wale waliotarajiwa kunufaika katika mgawo wa mwaka huu wa masomo.
Kutoka katika familia zenye uwezo kifedha ni miongoni mwa upungufu wa sifa uliowaponza wanafunzi hao 3,000 wa vyuo mbalimbali nchini.
Akizungumza na Nipashe jana, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, alisema mbali na kuondoa wanafunzi wasio na sifa ambao wote ni wa mwaka wa kwanza, wengine 87 ambao awali hawakujumuishwa kwenye orodha ya wanufaika kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya kusoma shule zisizo za Serikali, sasa watapata mikopo hiyo baada ya kubainika kuwa walisomeshwa na wafadhili.
Taarifa iliyotolewa na Badru mwishoni mwa wiki (Oktoba 30), ilikumbushia baadhi ya sifa muhimu za wanufaika wa mikopo kuwa ni wanafunzi yatima au walemavu; wanaotoka familia za hali duni kiuchumi hususani wale waliosoma kwenye shule za umma.
Alitaja kigezo kingine muhimu kwa wanufaika kuwa ni wanafunzi wanaosoma fani zilizo kwenye kipaumbele cha taifa, ambao ni wa fani za sayansi za tiba na afya; ualimu wa sayansi na hisabati na uhandisi wa viwanda, kilimo, mifugo, mafuta na gesi asilia. Fani nyingine za kipaumbele ni sayansi asili, sayansi ya ardhi, usanifu majengo na miundombinu.
Hivi karibuni, wakati akizindua hosteli za wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salam (UDSM), Rais John Magufuli aliitaka HELSB kuhakikisha kuwa mikopo inatolewa kwa wanafunzi wanaokidhi vigezo na siyo kinyume chake.
Rais aliwataja baadhi ya wenye sifa kuwa ni watoto watokao kwenye familia maskini na kusisitiza kuwa kamwe isitolewe kwa watu wa familia zenye uwezo kiuchumi wakiwamo watoto wa viongozi kama wa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako.
UFAFANUZI WALIOKOSA SIFA
Akifafanua zaidi juu ya wanafunzi waliokosa sifa na kuondolewa kwenye orodha, Badru alisema: “Kuna watu hawakugundua, katika ile batch (awamu) ya kwanza kulikuwa na makosa, tukarekebisha, tulivyorekebisha kuna watu waliondoka… kutokana na mfumo tuliotumia watu zaidi ya 3,000 waliondoka.”
Mkurugenzi huyo alisema kutokana na wanafunzi hao kuingizwa kimakosa kuwa kati ya watakaopata mikopo, bodi ilikuwa iwalipie kiasi kikubwa cha karo za masomo yao licha ya kuwa walikuwa hawana vigezo.
Hata hivyo, alisema mfumo huo umewapatia mikopo wanafunzi 87 ambao walikosa kutokana na kusoma katika shule binafsi kwa ufadhili kutoka katika taasisi mbalimbali.
Alisema wanafunzi wa kundi hilo walijaza fomu maalumu na baada ya kuingiza majina yao katika mfumo, walipatiwa mikopo.
Katika mwaka huu wa masomo, upangaji wa mikopo utategemeana na bajeti ya Sh. bilioni 483 zilizopitishwa na Bunge na kutarajiwa kunufaisha wanafunzi 119,012, kati yao 25,717 wakiwa ni wa mwaka wa kwanza na 93,295 wanaoendelea na masomo yao.
ONYO KWA WADAIWA SUGU
Katika hatua nyingine, Badru aliwataka wadaiwa sugu waliotakiwa kulipa mikopo kwa wakati, walipe mara moja kwa kuwa kuanzia wiki ijayo wataanza kuwafuatilia watu hao pamoja na wadhamini wao na kuwapeleka mahakamani.
Alisema kila aliyenufaika na mkopo wa elimu ya juu, anatakiwa kulipa kupitia namba za benki za bodi hiyo ambazo zinapatikana katika benki zote nchini.
“Kila aliyenufaika na mkopo wa elimu ya juu anatakiwa alipe kwa muda mwafaka… kuanzia wiki ijayo tutaanzisha operesheni ya kuwasaka wadaiwa sugu ambao walitakiwa kulipa na bado hawajalipa,” alisema Badru.
Alisema sheria iliyoanzisha bodi hiyo inawataka wanufaika wa mikopo kuanza kuirejesha miezi 12 baada ya kumaliza masomo.
“Tutawafikisha mahakamani. Sheria iko wazi, wanapaswa kurejesha fedha. Tunafahamu wapo ambao wanadai hawana ajira. Lakini sheria inataka mkopo lazima urejeshe baada ya miezi 12 baada ya kumaliza masomo,” alisema.
Alisema kutokana na sheria iliyoanzisha bodi ya mikopo, kuna haja ya wahusika wote kujitathmini na kuhakikisha wanalipa madeni yao kwa namna yoyote ili wengine wanufaike.
Kuhusu wanufaika waliomaliza madeni yao lakini wanaendelea kukatwa katika mishahara yao, Badru alisema changamoto hiyo ilitokana na mifumo ya kibenki kutorekebishwa.
Alisema kwa sasa mifumo inarekebishwa ili kuondokana na tatizo hilo na kwamba waliokatwa fedha kimakosa, watarejeshewa fedha zao.
Aliongeza kuwa kwa wale waliokatwa kimakosa wanatakiwa kwenda kwenye ofisi za bodi hiyo ili taasisi hiyo ijiridhishe na mwishowe kuwarudishia fedha zao.
Hivi karibuni, alipotembelea ofisi za Nipashe zilizopo Mikocheni jijini, Badru alisema sasa bodi hiyo inadai Sh. bilioni 14 ambazo zilikopeshwa kwa wanafunzi mbalimbali kabla ya kuanzishwa kwa chombo hicho mwaka 2005.
Kabla ya kuundwa kwa bodi hiyo, wanafunzi walikuwa wanakopeshwa fedha na wizara yenye dhamana ya elimu.
Alisema wakati huo, wanafunzi 38,000 walikopeshwa Sh. bilioni 51 na zaidi ya miaka 10 baadaye, wamelipa Sh. bilioni 36.
No comments:
Post a Comment
Subscribe My YouTube Channel Here:
https://www.youtube.com/channel/UCRdp...
Like My Facebook page:
https://www.facebook.com/lyizzmaker
Follow Me On Twitter:
https://www.twitter.com/habariyamjini
Follow Me on Instagram:
https://www.instagram.com/habariyamjini