Tuesday, 9 September 2025

KUTOKA MKAPA VS MREMA HADI SAMIA VS MWALIMU.


Bila shaka wanahistoria wanaendelea kukusanya takwimu za namna uchaguzi mkuu wa Tanzania 2025 huu utakumbukwa miaka ya mbeleni. Lakini hadi kufikia sasa, tayari kipo ambacho bila shaka hakitaachwa kutajwa.

Kwamba wakati wagombea wa chama cha tawala Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiendelea kuchanja mbuga kujinasibu kwa kile walichowafanyia Watanzania na kuwaahidi watakachowafanyia miaka mingine mitano ijayo, washindani tunaoweza walau kuwaita wa kiwango chao wanazunguka katika valanda za mahakama - mmoja akipigania kurejeshwa kwenye ulingo wa mapambano mwingine akipambana kupangua kesi ya uhaini, ambayo akikutwa na hatia itamgaharimu uhai wake.

Kwa miaka thelathini iliyopita, awamu sita za uchaguzi mkuu, nyakati kama hizi hali ilikuwa tofauti. Hata kwa uchaguzi wa kwanza kabisa baada ya kurejeshwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, mgombea wa chama tawala hakuteleza mithili ya kushuka mlima Kitonga mkoani Iringa, bali alipambana na mshindani aliyemtoa jasho kweli kweli.

Mkapa vs Mrema


Uchaguzi wa mwaka 1995 ulikuwa wa kwanza wa vyama vingi tangu ule wa Tanganyika mwaka 1958 kwa Tnzania Bara na mwaka 1963 kwa Zanzibar, enzi za ukoloni wa Uingereza na mwarabu mtawalia, na wenye vyama vinne tu vichanga vya upinzani. Lakini mgombea wa wakati ule wa CCM Benjamin William Mkapa alikuwa na kibarua cha kutosha.

John Momose Cheyo wa UDP na Profesa Ibrahim Haruna Lipumba wa CUF walipambana kwa namna yao, lakini ilikuwa mgombea wa NCCR Mageuzi Augustine Lyatonga Mrema aliyemtoa jasho Mkapa.

Ikiwa wewe si Gen Z, bila shaka utakumbuka mbwembwe za wafuasi wa Mrema. Kina mama walimtandikia kanga mtaani asikanyage vumbi, vijana walisukuma gari lake hata kama lilikuwa zima tu, alibebwa pia. Rangi za bluu, nyeupe na nyeusi zilitanda kama zilivyokuwa zimezagaa kijani na njano. Picha kubwa ya Mrema akiwa amevalia kibalagashea ilizagaa kuanzia kwenye nguzo za umeme hadi kwenye vifungishio vya vitumbua kwa mama lishe.

Mrema, aliyekuwa ameihama CCM chiniya miezi minane kabla ya kampeni za uchaguzi mkuu kuanza, aliachwa akitamba mtaani na kukichachafya chama chake cha zamani kwa shutuma nzito za kuifuga rushwa na kushindwa kuwaletea wananchi ili wawe na maisha bora. Mwishowe, Mkapa aliondoka na kura milioni nne sawa ana asilimia 61 huku Mrema akiwa na milioni moja na lake nane, sawa na asilimia 28 ya kura zote.

Mrema alifanikiwa kumtikisa Mkapa na CCM wakiwa na uungwaji mkono wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye si tu kwamba alikuwa na ushawishi mkubwa wa kisiasa Tanzania, 'hakupendelea' vyama vingi na alivikebehi wazi wazi. Hata hivyo, wote, Mwalimu na CCM waliheshimu ushiriki wao na kuwapa nafasi.

Baada ya misukosuko ndani ya NCCR Mageuzi, Mrema alitimkia TLP na hapo umaarufu wake ukashuka. Uchaguzi uliofuata miaka mitano baadaye (2000), Lipumba na chama chake cha CUF wakapanda na kuchukua nafasi ya NCCR Mageuzi. Hata hivyo mshike mshike wa uchaguzi ulihamia Zanzibar.

Katika uchaguzi uliotangulia wa mwaka 1995, CCM wakiongozwa na Dkt. Salmin Amour na upinzani CUF wakiwa na Maalim Seif Sharif Hamad walimenyana kweli kweli kiasi kwamba chama tawala kilishinda kwa asilimia 50 na zaidi kidogo tu. Wapinzani na wafuatiliaji wengine waliamini CUF ilishinda uchaguzi huo, lakini isivyo bahati walidhurumiwa.

Kikwete vs Lipumba





Uchaguzi wa mwaka 2000 sasa ukawa patashika nguo kuchanika, lakini kwa upande wa Zanzibar. Huko Bara, Chadema walimuunga mkono Lipumba wa CUF lakini macho yote yalikuwa Zanzibar. Baada ya uchaguzi, CUF ilipinga matokeo ya uchaguzi huu na kuipa muda serikali kuyatengua. Hata hivyo serikali ilikataa kufanya hivyo.

Kwanza wabunge na wawakilishi wa CUF wakagoma kuingia katika vyombo vya uwakilishi- hivyo majimbo yao yakatangazwa kuwa wazi. Uchaguzi mdogo ulipoitishwa, wafuasi wa CUF wakapiga kile kilichoitwa 'kura za maruani' kisha Januari 27, 2021 ikawaingiza wanachama wake barabarani na kauli mbiu ya 'Jino kwa Jino', huku ikiwahimiza vijana kuwa 'ngangari' (imara). Maandamano haya yakakutana na jeshi la polisi lililokuwa limejiandaa kuwakabili. Purukushani zilizofuata zilisababisha mauaji ya watu 35, kwa mujibu w CUF, lakini serikali ilishikilia kwamba ni watu 21 tu waliouawa. Baadhi walipata ulemavu, wengine waliikimbia nchi na mali za watu wengi ziliharibiwa.

Wanahistoria wanakubaliana kuwa uchaguzi huu uliitia doa jeusi historia ya demokrasia Tanzania. Mkapa ameandika katika kitabu chake cha "My Life, My Purpose" kwamba mauaji haya ndiyo doa kubwa zaidi katika kipindi cha urais wake, akitamka wazi kwamba muarobaini wa machafuko ya uchaguzi kama yale ni tume huru ya uchaguzi.

"Kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi itakayokubalika na vyama vyote kutachochea kuweka na kukuza demokrasia. Hii itasaidia kupunguza malalamiko, hali kadhalika vyama kuwa na Imani na chombo cha uchaguzi" anaandika Mkapa.

Matokeo ya uchaguzi yalipotoka, Mkapa alishinda kwa asilimia 71.7, Lipumba alishika nafasi ya pili kwa asilimia 16.3.

Mwaka 2005 CCM iliingiza damu mpya chini ya Jakaya Mrisho Kikwete. Akiingia na kauli mbiu yake ya Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya, Kikwete alikuwa na mvuto mkubwa kwa wapiga kura. Hata hivyo, aliingia wakati vyama vya upinzani pia vilikuwa vimeendelea kuimarika.


CUF kilikuwa na Profesa Ibrahim Lipumba, Chadema walikuwa na Freeman Mbowe, Augustine Mrema alipeperusha bendera ya TLP, mwanasiasa machachari Mchungaji Christopher Mtikila alikuwepo kwenye kinyang'anyiro kwa tiketi ya DP, huku Profesa Sengondo Mvungi akikiongoza chama cha NCCR Mageuzi.

Kikwete aliibuka na ushindi mnono wa asilimia 80.28 akifuatiwa kwa mbali na Lipumba aliyeambulia kura milioni 1.3 huku wagombea waliobaki wakigawana zilizokuwa zimesalia.

Wanazuoni mbalimbali, na hata wanasiasa wa upinzani wanakubaliana kwamba utawala wa Kikwete ulikuja na 'neema' iliyosaidia kukomaza vyama vya upinzani na ushiriki wa wananchi kwa ujumla. Japo mazingira hayakuwa mazuri kwa asilimia mia moja, vyama na wanasiasa walikuwa na ahueni ya uhuru wa kufanya shughuli za kisiasa huku kwa upande mmoja vyombo vya habari vikipewa walau nafasi kidogo kufanya kazi yake. Kwa upande mwingine mitandao ya kijamii nayo iliendelea kuchipuka.

Kikwete vs Slaa kule Magufuli vs Lowassa




Kuelekea uchaguzi wa 2010, Chadema ilikuwa imeiva kwa kiwango cha kuridhisha. Wakati huo pia rushwa ilikuwa imetapakaa kila kona ya nchi – kuanzia kashfa ya ufisadi wa kuchotwa fedha shilingi bilioni 133 kutoka akaunti ya madeni ya nje( EPA) hadi wa machimbo ya dhahabu ya Buzwagi. Hii ikawa ndiyo agenda kubwa ya Chadema waliyoingia nayo barabarani kwa mtindo wa kile walichokiita 'Operesheni Sangara'.

Awamu hii Kikwete alimenyana na Dkt. Wilbroad Slaa ambaye pia ndiye alikuwa kinara wa Oparesheni Sangara. Japo katika matokeo ya uchaguzi Dkt. Slaa aliambualia kura milioni mbili pekee, sawa na asilimia 26.34, Chadema ilivuna wabunge takribani 22, huku ikiongoza halmashauri kadhaa nchini. Kwa kanda ya ziwa, kwa mfano, Chadema ilichukua majimbo yapatayo kumi kati ya 43 ya wakati huo.

Kwa mshike mshike ambao Chadema iliwapa CCM katika opareshini yake hiyo au hata wakati wa kampeni za uchaguzi wenyewe, bila shaka utawala wa wakati ule ungeamua kupata kosa la uhaini katika kauli alizozitoa Dkt Slaa mshindani mkubwa wa Kikwete, bila shaka wasingeikosa.

Lakini badala yake, CCM ilijibu mshike mshike wa Chadema kwa kuanzisha kampeni yake yenyewe ya kujivua gamba iliyolenga kuwaengua viongozi wote wa CCM ambao aidha walikuwa wakishutumiwa kwa vitendo vya rushwa au hawakuwa wakichapa kazi kama chama na wananchi walivyotatarajia.

Japo figisu za hapa na pale dhidi ya upinzani hazikukosekana kabisa, ushindani wa jumla ukawa kati ya chama na chama katika kutafuta imani ya wananchi na si mabavu ya chama kimoja kukinyamazisha au kukiondoa kabisa chama kingine kisishiriki.

Baada ya Kikwete kuingia madarakani hakutafuta kuwanyoosha wapinzani, na kwa idadi kubwa ya wabunge ambayo wapinzani walikuwa wamevuna katika uchaguzi ulioisha, waliendelea kukua na kuimarika katika kuiwajibisha serikali ndani na nje ya bunge.

Lakini ni mchakato wa Katiba mpya ulioanza mnamo mwaka 2011 na kukwama mwaka 2014 ndiyo uliwaunganisha zaidi wapinzani kuelekea uchaguzi wa mwaka 2015.

Baada ya kususia mchakato huo, upinzani uliunda umoja waliouita Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) walioutumia si tu kuwaeleza Wananchi wasichokipenda katika mchakato huo wa katiba, lakini umoja huo pia ukawa ndiyo chombo walichoingia nacho uchaguzi wa 2015. Na mafarakano ndani ya CCM yakawaletea upinzani Edward Ngoyai Lowassa ambaye mara moja wakampa nafasi ya kuipeperusha bendera ya muungano huo wa upinzani.

Kuanzia mashindano ya kupiga push-up na majigambo ya mikutano ya nani inayojaza watu wengi, uchaguzi wa mwaka 2015 ulikuwa wa mshike mshike kuliko uchaguzi mwingine wowote tangu wa 1995.

Upinzani wakanufaika kwa kumpata mgombea ambaye si tu alitishia kukimega Chama Cha Mapinduzi lakini alikuwa na mvuto wa hali ya juu kwa mamilioni ya wapiga kura.

Kwa mara ya kwanza, upinzani ukafanikiwa kukokota asilimia arobaini ya kura za urais tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa. CCM kwa upande mwingine, mgombea wake John Pombe Magufuli, ikakusanya asilimia 58.4 ya kura, ikiwa ni kiwango cha chini zaidi kupata kutokea kwa mgombea urais wa Muungano kutipia CCM.

Samia vs Mwajuma au Samia vs Mwalimu



Magufuli hakuwa na uswahiba sana na wapinzani, akiwashutumu kutumika na mabeberu na kumchelewesha katika kazi zake, hadi aliapa kwamba kufikia mwaka 2020 atakuwa ameuua upinzani Tanzania. Ni wakati ambao upinzani ulikuwa taabuni na pengine kufanya ukawa taabani ukilinganisha na nguzu waliyokuwa nayo katika uchaguzi wa 2015 na hata 2010.

Pamoja na serikali yake kuleta kashkashi dhidi ya upinzani, uchaguzi wa mwaka 2020, chama kikuu cha upinzania Chadema kilifanikiwa kumsimamisha mgombea urais Tundu Antipas Lissu.

Akiwa amerejea nchini mahsusi kushiriki uchaguzi huo baada ya kuwa akipatiwa matibabu Ubelgiji kutokana na kushambuliwa kwa takribani risasi 16 miaka mitatu tu kabla, Lissu aliwavutia wapiga kura wengi kwa uwezo wake wa kuchambua mambo na kufafanua masuala mtambuka kwa njia rahisi kabisa. Magufuli kwa upande mwingine alijigamba kwa kazi ya kujenga miundo mbinu na kuanzisha miradi mikubwa mikubwa.

Upinzani ulipitia wakati mgumu sana katika uchaguzi huu ikiwa ni pamoja na mamia ya viongozi na wafuasi wao kuswekwa ndani kwa kesi zisizokuwa na dhamana, wengine waliripotiwa kuuawa huku wengine wakikimbia nchi kunusuru maisha yao. Lakini pamoja na misukosuko yote hii, upinzani ulishiriki na kuchangia katika kutia uchaguzi vuguvugu la ushindani. Hata hivyo Mara zote Serikali kupitia mamlaka zake, iliweka wazi kwamba, kila hatua iliyochukuliwa dhidi ya upinzani ama mpinzani ama chama cha upinzani, kilifuata sheria na hakukuwa na makusudi yoyote mabaya dhidi yao, ikiwemo kuenguliwa kwneye uchaguzi wa 2019 na ule wa 2020.

Imefika mwaka 2025, chama kikuu cha upinzani, Chadema hakishiriki, kwa sababu ya kutaka mabadiliko. Mgombea wake urais aliyepita na mwenyekiti wake, Tundu Lissu yuko ndani kwa kosa la uhaini. Chama kikuu cha pili kwa upinzani, ACT Wazalendo, mgombea wake Urais, Luhaga Mpina, ameenguliwa kwa kile kilichoeelezwa uteuzi wake kukiuka utaratibu na katiba ya chama hicho.

Kwa sasa CCM inatamba kutoka kona moja ya nchi hadi nyingine. Wagombea na vyama inavyoshindana navyo, havijaonyesha nguvu yake kwenye uchaguzi wowote katika miaka ya hivi karibuni.

Kwa mazingira haya, mgombea wa CCM Samia Suluhu Hassan anapambana na vyama vingine kumi na sita ambavyo jumla ya kura walizozipata katika uchaguzi uliopita ni 524,023, ambazo hazifikii hata nusu ya kura ilizopata Chadema katika ushindani ambao wagombea walipitia kila aina ya dhoruba katika kushiriki uchaguzi

Wakati mgombea wa Chadema alipata kura 1,933,271 katika uchaguzi uliopita, mgombea kutoka chama cha CHAUMMA wa wakati ule alipata kura 32,878. Katika uchaguzi huu, CHAUMMA, kinachoundwa na wafuasi wa Chadema waliotimkia huko baada ya uchaguzi wa ndani wa chama, ndicho chama kinachotarajiwa kukitoa jasho chama tawala.

Pamoja na upinzani kwenye uchaguzi mkuu wa sasa kuonekana na nguvu isiyo tisha na wengi kuhoji kwanini CCM mama anatumia nguvu sana wakati upinzani haupo? Mgombea wake, Rais Samia amewajibu mwishoni mwa wiki akiwa katika kampeni za uchaguzi akisema: "Waswahili wanasema anayedharau mwiba ukimchoma mguu unaota tende. Sasa usisubiri mpaka uchomwe na msumari, hata mwiba lazima uushughilkie".

Kwa kauli hii tafsiri yake ni kwamba, hata upinzani huu wa sasa kwenye uchaguzi wa mwaka huu unaoonekana usio na nguvu, hainaanishi chama chake na yeye kubweteka.

Bado kuna swali la kujiuliza ni yupi kati ya Salum Mwalimu wa CHAUMMA, Mwajuma Mirambo wa chama cha UMD, au Georges Gabriel Bussungu wa TADEA atakayemtia joto Samia? Tungoje tuone.

No comments:

Post a Comment

Subscribe My YouTube Channel Here:
https://www.youtube.com/channel/UCRdp...

Like My Facebook page:
https://www.facebook.com/lyizzmaker

Follow Me On Twitter:
https://www.twitter.com/habariyamjini

Follow Me on Instagram:
https://www.instagram.com/habariyamjini