Thursday, 18 September 2025

MGOMO WA KITAIFA WA VYUO VIKUU WAANZA KENYA.



Mgomo wa kitaifa wa vyuo vikuu nchini Kenya umeanza baada ya mazungumzo kati ya vyama vya wahadhiri na serikali kuvunjika.
Pande zote mbili zinailaumu Tume ya Kuratibu Mishahara na Marupurupu ya wafanyikazi wa umma kwa kukwamisha suluhu ya mzozo huo.

Wafanyikazi wa Vyuo Vikuu wanadai malimbikizi ya mishahara ya shilingi bilioni mbili za Kenya.
Matakwa ya vyama vya wahadhiri kutimizwa

Chama cha Wahadhiri wa Vyuo Vikuu nchini Kenya, UASU na Chama cha Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu nchini Kenya (KUSU) vimetangaza kuwa wahadhiri wamesitisha huduma zao hadi madai matatu ya msingi yatakapotimizwa:

Kutolewa kwa shilingi bilioni 2.73 kutoka Awamu ya Piliya mkataba wa maelewano ya pamoja wa mwaka 2021–2025 uliopaswa kulipwa Julai mwaka huu, kulipwa kwa deni la shilingi bilioni 7.9 la mkataba wa mwaka 2017–2021, na kuanza kwa mazungumzo na usajili wa mkataba mpya wa 2025–2029.

Katibu Mkuu wa UASU, Constantine Wasonga, ameilaumu Tume ya Kuratibu Mishahara ya Wafanyikazi wa Umma kwa kupuuza maagizo ya mahakama yaliyotaka fedha zitengwe kwa ajili ya mikataba hiyo ya CBA. Mgomo huo unatarajiwa kuvuruga masomo ya maelfu ya wanafunzi kote nchini, ikivihusisha vyuo vikuu takriban 45.

"Hatuwezi kusubiri kwa muda mrefu, lakini usishangae maanake tumeuzoea mchezo huu, hakuna mkataba wa maelewano katika vyuo vikuu ambao tumesaini bila kufanya mgomo. Sababu wanataka mgomo sasa tutacheza huo mchezo,” alisema Wasonga.

Dkt. Wasonga alikataa kikao cha mazungumzo kilichoitishwa Ijumaa na Jukwaa la Mashauriano la Baraza la Vyuo Vikuu vya Umma akikitaja kuwa ni mchezo wa kisiasa,wenye hadaa nyingi, akisema hakukuwa na mapendekezo madhubuti yaliyowasilishwa.

Alisema kuwa wahadhiri hawali kauli za nia na kuongeza kuwa wahadhiri hawali ahadi zisizo na utekelezaji. Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu ya Juu, Beatrice Inyangala, kwa upande wake, ameonyesha matumaini kuwa kumekuwa na maendeleo katika mazungumzo hayo.

No comments:

Post a Comment

Subscribe My YouTube Channel Here:
https://www.youtube.com/channel/UCRdp...

Like My Facebook page:
https://www.facebook.com/lyizzmaker

Follow Me On Twitter:
https://www.twitter.com/habariyamjini

Follow Me on Instagram:
https://www.instagram.com/habariyamjini