Thursday, 25 September 2025

SABABU RAMAPHOSA KUZIMIWA KIPAZA SAUTI AKIHUTUBIA UN.


Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amezimiwa kipaza sauti kwenye mkutano maalumu wa kujadili umuhimu wa kuanzishwa taifa huru la Palestina, baada ya kuelekeza mashambulizi dhidi ya Israel akidai inachofanya Gaza ni mauaji ya kimbari.
Pia, alifananisha mateso ya Wapalestina wanayofanyiwa na Israel na waliyoyapata Waafrika Kusini wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi wa makaburu nchini Afrika Kusini.

Ramaposa alizimiwa kipaza sauti ghafla kwenye mkutano maalumu ulioitishwa jijini New York na mataifa ya Ufaransa na Saudi Arabia, siku moja kabla ya kufanyika mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Akihutubia mkutano huo juzi jijini New York, Ramaphosa alisema suluhisho pekee la mgogoro wa Israeli na Palestina ni mataifa mawili yanalotegemea mipaka ya mwaka 1967. Ambapo mipaka hiyo ilianzishwa kwa lengo la kuanzisha nchi mbili ya Palestina na Israel, lakini lilianzishwa taifa moja tu la Israel.

Licha ya kutaka kusitishwa mapigano, kuachiliwa kwa mateka, na kuondolewa kwa vizingiti vinavyozuia utawala wa taifa la Palestina ikijumuisha ukuta wa kutenganisha wa Israel, alilinganisha mateso ya Wapalestina na historia ya ubaguzi wa rangi ya Afrika Kusini.

Katika shambulio lake la hasira dhidi ya Israel, ghafla kipaza sauti chake kilizimwa.

Mkutano wa Baraza Kuu

Hata hivyo, jana kwenye mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Ramaphosa kwenye hotuba yake alirejea mashambulizi yake dhidi ya Israel kwamba vitendo vyake huko Gaza ni mauaji ya kimbari na kuhimiza dunia itambue utawala wa taifa huru la Palestina.

Jana, Ramaphosa alisisitiza kuwa suluhisho pekee la mgogoro wa Israel na Palestina ni kuwapo mataifa mawili kwa kuangalia mipaka ya mwaka 1967, na akaomba kusitishwa kwa mapigano, kuachiliwa kwa mateka, pamoja na kuondolewa kwa vizingiti vinavyozuia utawala wa taifa la Palestina ikijumuisha ukuta wa kutenganisha wa Israel.

Ramaphosa alirejelea kesi ya Afrika Kusini mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki, akirudia mwelekeo wa dunia kuzungumzia vitendo vya Israel na amewataka wanachama wote wa Umoja wa Mataifa kulinda haki za Wapalestina na kusukuma suluhisho la mataifa mawili linalowezekana.

Alisema muda mfupi baada ya Umoja wa Mataifa kuanzishwa, Baraza Kuu lilipitisha Azimio Na. 181, lililopendekeza kuundwa kwa mataifa mawili ya Israel na Palestina.

Ramaphosa alisema baada ya kupitishwa kwa azimio hilo, ni taifa la Israel pekee lililoanzishwa, na kuwaacha Wapalestina wakiingia katika kipindi kirefu cha miaka mingi cha kutokuwa na taifa, kikielezewa na uvamizi wa muda mrefu na sasa mauaji ya kimbari.

“Afrika Kusini inasisitiza tena dhamira yake thabiti ya kuundwa kwa taifa la Palestina lenye mipaka inayoendelea, linaloishi kwa amani na kwa upande wa Israel, kulingana na mipaka ya mwaka 1967, na Jerusalem ya Mashariki kama mji mkuu wake.

“Wengi duniani wanapaswa kuendeleza azma hii licha ya juhudi za Israel za kufanya uanzishwaji wa taifa la Palestina kuwa jambo lisilowezekana,” alisema.

Ramaphosa alisema dunia imeshtushwa na ‘ukatili wa mauaji ya kimbari na uhalifu mkubwa wa kivita’ unaofanywa na Israel huko Gaza, unaolenga kuwaondoa kabisa Wapalestina katika kipande hicho kidogo cha ardhi, pamoja na upanuzi haramu wa makazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi.

Amesema hali hii imezidi kuwa mbaya zaidi kutokana na nia iliyo wazi ya Israel kutaka kutwaa kwa nguvu maeneo yote ya Palestina yaliyovamiwa.

“Uwezekano wa suluhisho la mataifa mawili unategemea kuheshimiwa kikamilifu na kwa usawa kwa sheria za kimataifa. Hili linahitaji utekelezaji wa haraka,” alisema.

Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao.

No comments:

Post a Comment

Subscribe My YouTube Channel Here:
https://www.youtube.com/channel/UCRdp...

Like My Facebook page:
https://www.facebook.com/lyizzmaker

Follow Me On Twitter:
https://www.twitter.com/habariyamjini

Follow Me on Instagram:
https://www.instagram.com/habariyamjini