Monday, 22 September 2025

UCHAGUZI TANZANIA 2025: AHADI TANO ZA WAGOMBEA URAIS ZILIZOZUA GUMZO.



Nianze kwa kukumbusha kilichotokea nchini Kenya katika uchaguzi wa 2022. Miongoni mwa wagombea wa kiti cha urais, kulikuwa na mtu akiitwa George Wajackoyah, ambaye ni wakili na profesa wa sheria, chini ya chama cha Roots.
Miongoni mwa ahadi zake zilizozua gumzo wakati wa kampeni za kusaka kura, ni kuinua uchumi wa Kenya kupitia kilimo cha bangi, ufugaji wa nyoka, kuuza nyama ya mbwa na fisi.

Aliamini kilimo cha bangi kitaleta suluhisho kwa matatizo ya uchumi wa Kenya, na changamoto za kifedha. Akinukuliwa na vyombo vya habari alisema:

“Tukilima bangi katika sehemu za Nyeri pekee, kila Mkenya atapokea kiasi cha shilingi za Kenya 200,000 kila mwaka. Tukilima bangi Nyeri pekee, tutajenga barabara pana na za kisasa mbili katika kila kaunti (Kenya ina kaunti 47), hatutaomba pesa wala kukopa madeni kutoka kwa nchi zingine.”

Sio tu kulima bangi pia aliahidi kuwaachilia huru wafungwa wote waliopatikana na hatia ya kulima, kusafirisha au kuuza bangi nchini humo. Fauka ya hilo, serikali yake itawalipa fidia ya shilingi milioni moja za Kenya baada ya kuwaachilia.

Aliahidi ufugaji wa nyoka ili kupata sumu itakayosafirishwa kwenda China na kutengeneza dawa za kutibu magonjwa ili Kenya kujipatia mapatano.

Alidai bei ya nyama ya mbwa na sehemu za uzazi wa fisi ni ghali sana nchini China, na utawala wake ungehakikisha Wakenya wanafuga mbwa kwa wingi ili kujinufaisha na soko la nyama hiyo na kuongeza ukuaji wa uchumi wa Kenya.

Miongoni mwa ahadi nyingine tata ni kutawala bila kutumia katiba, kufukuza raia wote wa kigeni wanaoishi Kenya bila kazi maalum na kuuwa watu wanaopatikana na makosa ya ufisadi.

Wakati uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 ukikaribia nchini Tanzania, na kampeni za uchaguzi zikizidi kushika kasi. Kumejitokeza baadhi ya ahadi ambazo kwa baadhi ya zimewaacha vinywa wazi:

‘Bwawa la Mamba Ikulu’



Akiwa katika mkutano wa kampeni jijini Dar es Salaam, mgombea wa urais kupitia Chama cha Alliance for African Farmers Party AAFP, Kunje Ngombale Mwiru ametoa hadi endapo atakabidhiwa mikoba ya urais wa Tanzania atachukua hatua kali dhidi ya mafisadi kwa kujenga bwawa kubwa la mamba katika Ikulu ya rais.


"Pale Ikulu nitachimba bwawa la mamba na wale mafisadi wote watadumbukizwa huko kuliwa hadi kuisha, na nguo zake mtazikuta zimewekwa hapo kama ushahidi wa hilo kujua kuna mtu alidumbukizwa humo.”


Amekazia ahadi yake kwa kusema, “pia, hiki kirungu changu nilichoshika mkononi kitatumika kuwapiga kabla hawajaingia ndani ya bwawa hilo na kama nina ziara nje ya nchi siku hiyo nitaiahirisha hadi nihakikishe nimemshughulikia fisadi huyo.”

‘Mabungo ni zaidi ya karafuu’



"Wazanzibari wajiandae kwa kilimo cha Mabungo, nitakapo kuwa rais lazima tuimarishe mashamba ya mabungo. Bungo ni tunda zuri, ni zaidi ya karafuu."

Hayo yamesemwa na Mgombea wa Urais wa Zanzibar kutoka Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA), Khamis Faki Mgau na kuongeza, "nikipata urais, ndani ya siku 30, sio siku 90 ni lazima watu wawajibike tuhakikishe tunapanda kilimo cha mibungo."

Bungo ni tunda la asili ya Afrika, linapatikana katika nchi kadhaa kama Tanzania, Comoro, Madagascar kuzitaja kwa uchache. Lina utajiri wa Vitamini C, hivyo lina faida zake kwa afya, lakini hakuna taarifa zinazoonesha kwamba lina soko kubwa kwa sasa kuizidi karafuu.

Bila shaka itakuwa kazi ya Mgau kuwa muasisi wa soko la mabungo kimataifa ikiwa ataingia Ikulu.

‘Kilimo cha Bangi’



Mgombea wa Urais kutoka visiwani Zanzibar, Said Soud Said kutoka Chama Cha Alliance For African Farmers Party, ameahidi ataruhusu kilimo cha bangi.

"Vijana katika nchi hii watalima vilimo mbalimbali vyenye tija, ikiwemo bangi. Bangi italimwa hapa na itauzwa nchi za nje kama zao la biashara. Nawahidi vijana, nikipata serikali watalima bangi na serikali itanunua na kusafirisha Ulaya, kupata pesa za kigeni ili kuondoa matatizo yetu. Tutalima kilimo cha biashara kwa nidhamu."

Ahadi hii imezua mjadala kwa sababu bangi ni zao haramu kisheria katika nchi nyingi duniani ikiwemo Tanzania, linapigwa marufuku kwa sababu ya athari zake kiafya, lakini yapo mataifa yanayoruhusu uzalishaji wa bangi kwa sababu ya matumizi ya dawa.

Mpaka kufikia Oktoba 2024, nchi 9 za Kiafrika tayari zimehalalisha kilimo cha bangi kwa ajili ya matumizi ya viwandani na dawa kwa mujibu wa mtandao wa habari za biashara wa Business Insider.

‘Ubwabwa kabla ya dripu’



Katika uzinduzi wa kampeni ya Chama cha Umma (CHAUMMA), mgombea mwenza wa urais Devotha Minja ameweka ahadi kwa wagonjwa kupatiwa ubwabwa wakifika hospitali hata kabla ya dripu.

"Sisi CHAUMMA sera yetu ni chakula, mgonjwa akifika hospitali badala ya kukutana na dripu anakutana na ubwabwa, anapiga ubwabwa anashushia na dawa."

Ubwabwa ni sera ya muda mrefu ya chama hicho. Katika kampeni za uchaguzi wa 2020, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ilipiga marufuku CHAUMMA kulisha watu ubwabwa katika mikutano ya kampeni, ikisema hiyo ni rushwa kwa wapiga kura.

Kwa sasa CHAUMMA wamebadili mbinu, wakiingia Ikulu ubwabswa utakuwepo hospitali – ule, ushibe kabla ya dripu.

“Posho 500,000 kila mwezi”



Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha Makini Ameir Hassan Ameir ametoa ahadi ya kutoa posho ya laki tano (USD 200) kwa kila Mzanzibari kwa kila mwezi mara tu baada ya kula kiapo cha kuwa Rais wa Zanzibar


Amesema mbali na kutoa posho hiyo amewahakikishia wananchi kuwa mshahara wa mtumishi wa serikali kima cha chini ni kuanzia shilingi Milioni Moja na Laki tano (1,500,000), ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuinua ustawi wa wananchi na kuboresha maisha yao.

Miongoni mwa waliotoa maoni yao katika mitandao ya kijamii kuhusu ahadi hii, wamenukuu msemo wa Waingereza - too good to be true (livutialo sana lina walakini). Nami nitasema, kwa vile uchaguzi haujafanyika na hajaingia Ikulu, hatuna haja ya kumaliza maneno. Tusubiri!

Kuna ile kasumba kwamba wanasiasa husema chochote tu ili wapate kura. Ahadi hizi zimezua gumzo kwa sababu baadhi zina ugumu katika kuzitekeleza, hasa ukizingatia kuwa wengi wao hawaelezi kinaga ubaga watafanikishaje ahadi zao na nyingine zina uhitaji kwa mabadiliko makubwa ya kisheria ili zitekelezwe.

Tukimaliza hapa, tusubiri ahadi nyingine, Oktoba 25 bado ni mbali.

No comments:

Post a Comment

Subscribe My YouTube Channel Here:
https://www.youtube.com/channel/UCRdp...

Like My Facebook page:
https://www.facebook.com/lyizzmaker

Follow Me On Twitter:
https://www.twitter.com/habariyamjini

Follow Me on Instagram:
https://www.instagram.com/habariyamjini