
Lakini, mabosi wa timu hiyo bado wanampa sapoti kocha huyo licha ya matokeo ya kichapo katika mechi ya mahasimu dhidi ya Manchester City.
Imeelezwa kwamba baadhi ya mastaa kwenye kikosi hicho hawafurahishwi na mtindo wa kucheza na mabeki wa kati watatu, mfumo ambao kocha huyo amekuwa akisisitiza utumike.
Man United imekumbana na kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa chama hilo la Pep Guardiola uwanjani Etihad, hivyo kuifanya kuwa na pointi nne tu katika mechi nne za Ligi Kuu England.
Na huo ni mwanzo wa hovyo zaidi kwenye Ligi Kuu England tangu mwaka 1992, huku timu hiyo ikitupwa nje pia kwenye michuano ya Kombe la Ligi - tena na timu ya League Two, Grimsby.
Amorim alisema baada ya mechi hiyo kwamba hatabadili staili yake ya uchezaji ya kumtumia fomesheni ya 3-4-2-1 licha ya kwamba haionekani kufanya vizuri Man United.
Aliongeza kwamba mabosi wa Man United watakachofanya ni kumwondoa kazini kama wataona staili hiyo si njia sahihi ya kuwafikisha kwenye malengo.
Kinara wa mabao wa Man United, Wayne Rooney alifichua kutazama mechi hiyo ya Manchester derby akiwa sambamba na wachezaji wenzake wa zamani.
Na kwenye orodha hiyo ya mastaa hao wa zamani wa Man United hakuna hata mmoja aliyekuwa anaelewa Man United inacheza kitu gani uwanjani, huku Rooney akisisitiza hali ya timu hiyo inazidi kuwa mbaya chini ya Amorim.
Baadhi wa mastaa waliopo kwenye kikosi hicho kwa sasa nao wameweka mashaka makubwa katika mtindo huo wa kiuchezaji wa kocha wao, licha ya kwamba bodi bado haijamwambia kuhusu suala la kubadilika.
Kinachoelezwa ni kwamba mabosi wakubwa wa klabu hiyo ya Man United bado wanampa sapoti Amorim, akimpatia muda wa kutosha kuona kama ataweka mambo sawa.
Mmiliki mwenza, bilionea Sir Jim Ratcliffe alionekana uwanjani Etihad wakati wa mechi hiyo, ambapo picha zilimwonyesha mikono ikiwa kichwani kwa masikitiko ya kile alichokuwa akikiona kwenye mechi hiyo, ambapo Phil Foden na Erling Haaland walitikisa nyavu.
Tajiri Ratcliffe aliifungua pochi kumpa Amorim pesa ya kusajili mastaa wapya, ambapo kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi miamba hiyo ilitumia Pauni 220 milioni kunasa mastaa.
Hivyo, kumfuta kazi kocha huyo mwenye umri wa miaka 40 ina maana kutahitajika kufanya maboresho mengine kwenye kikosi.
Lakini, Wayne Rooney alisema: “Wote tumeona, wote tulikuwa tunapata shida kuona ni kitu gani Man United inacheza. Mfumo ni upi? Kila mtu alishindwa kupata majibu, wote tulicheza soka kwenye kiwango kikubwa sana, hivyo tulikuwa kwenye wakati mgumu kuona kilichokuwa kinaendelea. Sidhani kama kuna yeyote anayeelewa na kukiamini kinachoendelea.
“Baada ya mwaka jana wakati Erik ten Hag alipofukuzwa na kuletwa Ruben, tulisikia timu itakavyocheza na kwamba mambo yatabadilika. Nadhani kama kocha akitaka ukweli wa moyo wake, mambo yamekuwa mabaya zaidi.”
Amorim amevuna pointi 31 tu katika mechi 31 alizoingoza Man United tangu alipotua Old Trafford katikati ya Novemba, amepoteza mechi 16 kati ya hizo. Msimu uliopita timu hiyo ilimaliza nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England na ilichapwa kwenye fainali ya Europa League dhidi ya Tottenham Hotspur, hivyo haipo kwenye michuano yoyote ya Ulaya msimu huu, ikiwa ni mara ya pili tangu Sir Alex Ferguson alipostaafu mwaka 2013.
Kocha Amorim mwenyewe anafahamu wazi presha kwa upande wake itazidi kupanda kama matokeo mazuri hayatapatikana, aliposema: “Hii si rekodi inayotakiwa hapa Man United.”
Man United inakabiliwa na mechi ngumu Jumamosi, ambapo itakabiliana na mabingwa wa dunia, Chelsea kipute kitakachopigwa huko Old Trafford. Taarifa ya klabu ilikanusha taarifa za wachezaji wa timu hiyo kupoteza imani na kocha Amorim na kwamba kinachoaminika ni kwamba kocha huyo bado anapewa sapoti na wachezaji wake kwenye vyumba vya kubadilishia.
No comments:
Post a Comment
Subscribe My YouTube Channel Here:
https://www.youtube.com/channel/UCRdp...
Like My Facebook page:
https://www.facebook.com/lyizzmaker
Follow Me On Twitter:
https://www.twitter.com/habariyamjini
Follow Me on Instagram:
https://www.instagram.com/habariyamjini