Wednesday, 17 September 2025

LISSU AGOMA, ATAKA WANACHADEMA WARUHUSIWE KUINGIA MAHAKAMANI.

 

Mvutano waibuka kwenye Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Dar es Salaam baada ya Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu kugoma kuendelea na shauri la uhaini akishinikiza wafuasi wa chama chake waruhusiwe kuingia mahakamani. Vuta nikuvute imeshuhudiwa kwenye Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Dar es Salaam nchini Tanzania baada ya Lissu kuiomba mahakama iahirishe kesi hiyo hadi pale wafuasi wake watakaporuhusiwa. Leo Jumanne Lissu anatarajia kutoa sababu ya pili ya pingamizi lake dhidi ya kesi ya uhaini, linaloegemea uhalali wa mahakama hiyo kusikilizia kesi yake.

Iliwalazimu majaji kuahirisha shauri la Mwenyekiti huyo wa CHADEMA kwa saa nzima baada ya mvutano mkali. Hata wanachama wachache wa CHADEMA walioingia kwenye ukumbi wa mahakama hiyo walilazimika kutoka nje baada ya kubaini kuwa wenzao wamezuiwa.
Kesi yaanza kusikilizwa baada ya mashauriano


Majira ya saa 5 asubuhi, kesi ilianza na katika hatua ya usikilizwaji ambapo Lissu atatoa sababu ya pili ya pingamizi lake, kuhusu uhalali wa mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo.

Siku ya Jumatatu, kabla ya Lissu kupanda kizimbani, vurugu zilizuka baina ya wafuasi wa CHADEMA na polisi ambapo askari wa usalama waliwajeruhi baadhi ya wanachama wa chama hicho. Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alipotoa ufafanuzi kuhusu vurugu hizo alitahadharisha kuwa kitendo chochote cha kuwachokoza askari walio kwenye majukumu yao, kitashughulikiwa haraka.

Ufafanuzi huu hata hivyo umepokelewa kwa hoja mchanganyiko, baadhi wakihoji kuhusu uhalali wa polisi kuwapiga raia lakini wengine wameunga mkono hoja ya Muliro.

Lissu amesema hati ya mashitaka dhidi yake ina mapungufu makubwa. Anahoji ni chapisho gani hasa kuhusu matamshi yake linatakiwa liwasilishwe, ama liwe kwa aina ya barua, barua pepe au chapisho jingine na kusisitiza watu wanaodaiwa kupokea taarifa hizo walipaswa kutajwa kisheria, vinginevyo hati hiyo inabaki kuwa na kasoro kubwa isiyoweza kurekebishwa.

No comments:

Post a Comment

Subscribe My YouTube Channel Here:
https://www.youtube.com/channel/UCRdp...

Like My Facebook page:
https://www.facebook.com/lyizzmaker

Follow Me On Twitter:
https://www.twitter.com/habariyamjini

Follow Me on Instagram:
https://www.instagram.com/habariyamjini