Tuesday, 23 September 2025

OUSMANE DEMBELE ATWAA TUZO YA BALLON D'OR 2025.


PARIS, UFARANSA: BAADA ya maswali ya muda mrefu juu ya nani atashinda tuzo ya Ballon d'Or mwaka huu, hatimaye majibu yamepatikana na staa wa Paris Saint-Germain, Ousmane Dembele ameshinda tuzo hiyo.

Dembele ameshinda tuzo hiyo kwa kuwabwaga mastaa wa Barcelona Lamine Yamal na Raphinha ambao pia walikuwa wanapewa nafasi kubwa.

Staa huyu wa kimataifa wa Ufaransa alionyesha kiwango bora sana msimu uliopita ambapo alicheza mechi 59, akafunga mabao 37 na kutoa asisti 14.

Katika msimu huo alishinda tuzo ya mchezaji bora wa msimu wa Ligue 1, mfungaji bora wa Ligue 1 na mchezaji bora wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Vilevile aliisaidia PSG kushinda taji la Ligi ya Mabingwa, Ligi Kuu Ufaransa, Coupe de France na French Super Cup.

Mbali ya tuzo hiyo iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu, katika upande wa tuzo ya kipa bora Gianluig Donnarumma alichaguliwa kuwa kipa bora.

Donnarumma ambaye kwa sasa anaichezea Manchester City, ameshinda tuzo hiyo kutokana na kiwango bora alichoonyesha msimu uliopita ambapo alisimama katika milingoti mitatu wakati PSG ikifanikiwa kushinda mataji matatu msimu uliopita ikiwemo Ligi ya Mabingwa pamoja na kufika fainali ya Kombe la Dunia kwa klabu.

Vilevile kocha wa PSG, Luis Enrique alichaguliwa kuwa kocha bora naye kutokana na kiwango hora ambacho PSG ilikionyesha msimu uliopita ikiwa chini yake.

Staa wa Barcelona, Lamine Yamal alishinda tuzo ya mchezaji bora kijana kwa mara yapili mfululizo baada ya kushinda pia mwaka jana.

Watu wengi walikuwa wakimshindanisha na Ousmane Dembele wakiamini alikuwa na nafasi kubwa ya kushinda tuzo ya mchezaji bora wa kiume wa mwaka kutokana na kiwango alichoonyesha akiwa na timu ya taifa ya Hispania mwaka jana ambapo aliisaidia kushinda taji la Euro, pia kiwango alichoonyesha akiwa na Barcelona.

Straika wa Arsenal, Viktor Gyokeres alishinda tuzo ya mfungaji bora baada ya kufunga mabao 54 katika mechi 52 za michuano yote akiwa na Sporting Lisbon msimu uliopita.

No comments:

Post a Comment

Subscribe My YouTube Channel Here:
https://www.youtube.com/channel/UCRdp...

Like My Facebook page:
https://www.facebook.com/lyizzmaker

Follow Me On Twitter:
https://www.twitter.com/habariyamjini

Follow Me on Instagram:
https://www.instagram.com/habariyamjini