Tuesday, 23 September 2025

SIMBU ATUA KISHUJAA, GWARIDE LIKIFUATA.


MWANARIADHA Alphonce Felix Simbu ametua nchini usiku wa kuamkia leo saa 9:00 alfajiri kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), akibeba medali ya dhahabu aliyonyakua kwenye mashindano ya Dunia ya Riadha yaliyofanyika Tokyo, Japan.
Simbu ambaye ameweka historia kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kushinda kwenye mbio za marathon, alipokelewa kwa shamrashamra na mamia ya mashabiki wamejitokeza kumpongeza ikiwemo familia yake.

Akizungumza mara baada ya kutua, Simbu amesema: “Nimefurahi kwa sababu Watanzania wengi wamejitokeza kwa ajili ya mapokezi haya. Niseme kuwa medali hii ni kwa ajili ya Watanzania wote. Hii ni hatua kubwa na furaha kwetu sote. Ushindi huu unadhihirisha kwamba mchezaji yeyote wa Kitanzania anaweza kufanya lolote katika mashindano yoyote ya kimataifa.”

Simbu ameongeza kuwa ushindi wake unapaswa kuwa chachu kwa wanariadha na wachezaji wa michezo mingine nchini akiwatia moyo wasikate tamaa.

“Kwa mchezo wa riadha hata mashindano yawe makubwa kwa kiasi gani, ukitia juhudi na ukajiandaa, unaweza kushinda. Sio rahisi, lakini kujituma kunasaidia sana. Niwasihi wachezaji wa Kitanzania kuamini kuwa wanaweza,” amesema.

Katika mashindano hayo yaliyofanyika mjini Tokyo, Simbu alishinda kwa staili ya aina yake kwa tofauti ndogo zaidi katika historia ya marathon ya dunia. Alimshinda Mjerumani Amanol Petros kwa sekunde 0.03.

Simbu na Petros walimaliza kwa muda sawa wa saa 2:09:48, lakini teknolojia ya picha ilionyesha Mtanzania huyo ndiye aliyeingia mstari wa mwisho kwanza. Muitaliano Iliass Aouani alishika nafasi ya tatu kwa muda wa saa 2:09:53.

Ushindi huo ulimpandisha chati kutoka medali ya shaba aliyoshinda London mwaka 2017 hadi dhahabu, huku akitimiza ndoto aliyoiweka kwa zaidi ya miaka 10.

“Hii medali nimeitafuta kwa miaka 10. Mara ya kwanza nilishiriki mwaka 2015 China nikakosa, 2017 London nikapata shaba, nikaendelea kujaribu na kukosa, lakini sikukata tamaa. Niliapa kujaribu tena na tena. Hata Wakenya walishangaa kuona Mtanzania akishinda,” amesema Simbu.

Baada ya kutua nchini mwanaridha huyo anatarajiwa kuwa na gwaride la mapokezi ambalo litaanza asubuhi hii ya Jumanne kutoka Vinguguti katika hoteli ya Blue Sapphire (Vingunguti ambako alikwenda kupumzika kwa muda) kupitia barabara ya Nyerere na kuelekea Tazara, Buguruni, Karume, Kariakoo na kumalizia Posta.

No comments:

Post a Comment

Subscribe My YouTube Channel Here:
https://www.youtube.com/channel/UCRdp...

Like My Facebook page:
https://www.facebook.com/lyizzmaker

Follow Me On Twitter:
https://www.twitter.com/habariyamjini

Follow Me on Instagram:
https://www.instagram.com/habariyamjini