Tuesday, 23 September 2025

MAHAKAMA KUU TANZANIA YATUPILIA MBALI MAPINGAMIZI YA LISSU.



Mahakama Kuu nchini Tanzania imetupilia mbali mapingamizi yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu kuhusu makosa aliyoyabaini katika hati ya mashitaka na hitilafu katika viambatanisho vya hati ya mashitaka.
Amegonga mwamba tena. Hivyo ndivyo tunavyoweza kusema baada ya mahakama kuu masijala ndogo ya Dar es Salaam, kuyatupilia mbali mapingamizi yaliyowekwa na Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, katika kesi ya uhaini inayomkabili.

Mara baada ya kesi hiyo kupelekwa Mahakama Kuu na kisha mwanasiasa huyo kusomewa mashitaka, alibainisha mapungufu katika maeneo ya kesi hiyo ikiwamo kukosewa kwa hati ya mashitaka, hitiflafu katika viambatanisho vya hati ya mashitaka, mamlaka ya mahakama kuu na kesi hiyo na utata katika maelezo ya mashahidi.

Hata hivyo baada ya mapingamizi mawili ya awali kugonga mwamba, mahakama imeyatupilia mbali mapingamizi yaliyotolewa na Lissu, la kwanza hitilafu katika hati ya mashitaka na la pili ni hoja ya Lissu kuwa viambatanisho vya hati ya mashitaka vipo kinyume na sheria.

Pamoja na hayo, Mahakama imeikataa hoja ya Lissu kutaka kesi hiyo iendeshwe katika mahakama ya wazi ikiwamo kurusha kesi hiyo mubashara ambapo Mahakama imeamua kuwa tayari mahakama hiyo ni ya wazi lakini kwa kuwa kuna mashahidi wanaopaswa kulindwa, mwenendo wa kesi hauwezi kurushwa mubashara.

Baada ya uamuzi huo, mahakama iliendelea kwa upande wa Jamhuri kusoma maelezo ya awali ya kesi hiyo na jaji alimsomea mashitaka yake.


No comments:

Post a Comment

Subscribe My YouTube Channel Here:
https://www.youtube.com/channel/UCRdp...

Like My Facebook page:
https://www.facebook.com/lyizzmaker

Follow Me On Twitter:
https://www.twitter.com/habariyamjini

Follow Me on Instagram:
https://www.instagram.com/habariyamjini